Halmashauri ya Mvomero imeanza kufanyiwa tathimini ya mapato ya biashara ya Kaboni

Halmashauri ya Mvomero wajivunia kupata elimu ya Mapato yatokanayo na biashara ya Kaboni kutoka kwa watafiti wa Chuo kikuu cha Sokoine Cha Kilimo, SUA na Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni, NCMC.

Akizungumza na SUAMEDIA Afisa Misitu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, Bi Lily Haule amewapongeza watafiti hao kwa kufika Kijiji cha Masimba, Kata ya Pemba. Lengo la watafiti hao ni kufanya tathmini ya mapato ya Kaboni kama njia endelevu ya uwezeshaji kifedha katika uhifadhi na usimamizi wa misitu ya jamii.

Bi Lily ameeleza kuwa biashara ya Kaboni itachangia kwa kiasi kikubwa usimamizi endelevu wa misitu ya jamii katika Wilaya ya Mvomero.  Sababu biashara hiyo ya kaboni inatarajiwa kuleta mapato ambayo yanaweza kutumika kwenye maendeleo ya jamii na kupunguza utegemezi kwa Halmashauri na Serikali kuu.

“Nianze kwa kusema tafiti ndizo huleta maendeleo katika nchi, biashara hii kama ikiwa chanya itampunguzia bajeti Mkurugenzi kwa maana mapato yatakayo patikana katika biashara hii yatatumika katika kuleta maendeleo vijijini” amesema Bi Lily.

Bi Lily Ameongeza kuwa kama Halmashauri imeongezewa ari kupitia wananchi wake kwa kuweza kusimamia rasilimali za misitu wenyewe kwa moyo pasipo kutegemea wataalam wengine sababu kupitia elimu waliyoipata wanakijiji imewaonesha faida ya biashara ya Kaboni katika maeneo yao.

Diwani wa Kata ya Pemba Mheshimiwa Coster Peter Reuben amewaasa wananchi wake kuendelea kutunza misitu iliyopo katika eneo la Masimba na kujivunia kuwa sehemu ya eneo lililochaguliwa na kufanyiwa tafiti yenye ustawi kwa kata yao ya Pemba. “Biashara ya kaboni nzuri na baadhi ya maeneo ya nchi wameshapata mafanikio na wataendelea kuona mafanikio maana sasa wataalam katika sekta hiyo wamekuja na wanafanya tathimini ya mapato ya kaboni kama njia endelevu ya usimamizi wa misitu ya jamii” Amesema Mh. Coster.

Pia ametolea mfano wa Halmashauri ya Tanganyika iliyopo mkoa wa Katavi kwa kupata mapato makubwa kupitia biashara hiyo ya Kaboni kwa kujipatia takribani Bilioni 6.

Kwa upande wao wananchi wa kijiji cha Masimba wameonesha kufurahia ujio wa mradi huo wa utafiti na kuwaomba waendelee kuwafikia mara kwa mara. Huku wakionesha dhamira yao ya kupata mapato zaidi kwaajili ya kujenga Shule na Zahanati. Wametoa mifano ya matokeo Chanya yaliyotokana na usimamizi bora wa misitu ikiwemo kujenga shule ya kata.

Dkt. Paulo J. Lyimo ambaye ni Mtafiti na Mhadhiri katika Chuo kikuu cha Sokoine Cha Kilimo, SUA na Afisa Mwandamizi kutoka Kituo cha Taifa cha Kuratibu Kaboni, NCMC amesema kuwa katika tathimni waliyoifanya imeonesha kuwa uelewa wa biashara ya Kaboni bado upo chini kwa viongozi wa Kijiji na wananchi wake.

Dkt. Kajenje Magessa ambaye ni mtafiti mkuu katika mradi huo na pia Mhadhiri wa SUA ameeleza lengo la kukutana na wanakijiji, uongozi wa kijiji pamoja na maafisa wa misitu ni kutathimini uelewa wao juu ya usimamizi wa misitu ya jamii na biashara ya Kaboni. Pia amewapongeza viongozi wa Kijiji na wananchi kwa ujumla kwa ushirikiano waliouonyesha wakati wa kufanya tathimini.

Dkt. Magessa amewashukuru wafadhili wa mradi ambao ni Idara ya Mazingira Chakula na Masuala ya Vijijini ya Uingereza (Department for Environment, Food and Rural Affairs (Defra) of United Kingdom) kwa ushirikiano na Idara ya Kimataifa ya Maendeleo ya Serikali ya Uingereza na Shirika la maendeleo mbadala (Development Alternatives, Inc. (DAI). Na pia amekishukuru Chuo Kikuu cha Bangor cha nchini Uingereza kwa kukubali kushirikiana na watafiti wa SUA kutekeleza mradi huu. Aidha ametoa  shukrani za pekee kwa Rais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kuwa msitari wa mbele kuunga juhudi za Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo katika  uhifadhi kwa manufaa ya nchi.